SWALI NA. 1: Je maziwa yapi ni bora zaidi kwa mtoto wangu? Ni ya mama au ya kopo?


JIBU: Maziwa ya mama ni bora kuliko kitu kingine cho chote kwa kuwa:

Maziwa ya kopo siyo sawa na ya binadamu. Ni kazi kuyatayarisha na hayana virutubisho kama maziwa ya mama. Ni chanzo cha magonjwa kama ya kuharisha.
MAZIWA YA MAMA NDIYO BORA KWA MTOTO WAKE

 



SWALI NA. 2: Je maziwa ya mama ya mwanzo ni mazuri kwa mtoto?

JIBU: Ndiyo. Ni mazuri sana. Maziwa haya kwa lugha ya kizungu yanaitwa Colostrum. Maziwa haya ni mazito, yenye rangi ya njano. Ni muhimu mtoto anyonye maziwa haya kwani yamejaa kinga za asili zitakazosaidia kumzuia mtoto asipate magonjwa hasa ya kuharisha na kifua.

 

 

 

 

 

 




SWALI NA. 3: Je mama mjamzito akishajifungua tu mtoto wake ampe nini cha kumuonjesha hapa duniani, chumvi au sukari?

JIBU: Mama mjamzito anapojifungua tu, cha kumuonjesha mtoto wake si chumvi wala sukari, bali ni maziwa yake mwenyewe. Maziwa ya mama yana kila kitu, yaani chumvi na sukari humo humo. Ni safi, ni fresh, yana usalama, yana viini vya kukinga mwili, yana joto linalomfaa mtoto na hayamletei mtoto kuharisha. Zawadi kubwa ambayo mama anatakiwa kumpa mtoto wake mchanga ni moja tu, nayo ni maziwa yanayotoka ndani ya ziwa lake mwenyewe. Na ampe ziwa hilo kuanzia mara tu anapozaliwa mtoto. Hakuna sababu yoyote ya kumchelewesha mtoto kunyonya ziwa.

 

 

 

 

 



SWALI NA. 4: Je mtoto anatakiwa aanze kunyonyeshwa tangu lini? Mbona mimi maziwa yangu yalichelewa sana kuanza kutoka na nikamwonea huruma mwanangu nikampa maji? Je nina upungufu gani mwilini mwangu?

JIBU: Mtoto anatakiwa aanze kunyonyeshwa maziwa ya mama mara tu anapozaliwa. Hakuna ulazima wowote wa kuchelewesha kitendo cha kumpa mtoto ziwa la mama yake.
Maziwa yako yalichelewa kutoka kwa vile hukumpatia mtoto ziwa mara tu alipozaliwa. Kitendo cha mtoto kunyonya huwa ndiyo msisimko kwa mama kutoa maziwa. Hakuna haja ya kumpa mtoto maji, kwani yatamfanya mtoto ajisikie kutosheka na hivyo asinyonye, na kutonyonya huko ndiko kunakosababisha maziwa yasitoke. Narudia tena, wewe huna upungufu wowote mwilini, ila huenda ulichelewa kumpa mtoto ziwa lako.

 

 

 

 




SWALI NA. 5: Je mtoto mdogo anayenyonya maziwa ya mama tu anasikia kiu?

JIBU: Mtoto mdogo anayenyonya maziwa ya mama tu yaani mtoto aliye na umri chini ya miezi 6 hahitaji maji ya kunywa. Maziwa ya mama yana maji ya kutosha hata wakati wa joto kali. Mtoto mchanga hahitaji maji ya kunywa mpaka afikishe miezi mine hata zaidi.

 

 

 

 

 

 

 

 



SWALI NA. 6: Je kuna utaalam maalum wa kuwanyonyesha watoto wachanga?

JIBU: Hakuna utaalamu maalum wa kuwanyonyesha watoto wachanga, kila mama anaweza kumnyonyesha mtoto wake. Hakikisha kuwa mtoto anapatiwa ziwa la mama yake mara tu anapozaliwa. Pasiwe na kisingizio cha mama kutokuwa na maziwa kwani kule kunyonyesha ndiko kunakomfanya mama atoe maziwa. Mtoto anyonye mara nyingi kiasi atakachopenda mwenyewe, asiwekewe vipimo. Hata wakati wa usiku mtoto asinyimwe kunyonya. Yote hayo ni mambo yanayoweza kuzingatiwa na mama yeyote na hatuwezi kusema kuwa yanahitaji utaalam maalum.

 

 

 

 

 

 



SWALI NA. 7: Mwanangu akinyonya maziwa yangu anaharisha, Je maziwa yangu yameharibika? Kama yameharibika nifanye nini ili yawe safi?

JIBU: Maziwa hayawezi kuharibika yakiwa ndani ya titi la mama. Kama mtoto wako anaharisha labda kuna sababu nyingine lakini siyo maziwa ya mama. Maziwa ya ng’ombe au ya kopo ndiyo yanayoweza kusababisha mtoto kuharisha. Vile vile mtoto akiwa na ugonjwa kama vile malaria anaweza kuharisha. Inafaa chanzo cha mtoto kuharisha kitafutwe kwa makini na ikiwezekana ushauri upatikane kutoka kwenye kituo cha afya. Ni muhimu ieleweke kwamba maziwa ya mama pekee hayamfanyi mtoto aharishe.

 

 

 

 




SWALI NA. 8: Kama mtoto wangu ananyonya vizuri, ninatakia nianze lini kumpa vyakula vingine kwa mfano uji na kadhalika?

JIBU: Umri wa kumpa mtoto vyakula vingine, yaani vyakula vya Kulikiza ni miezi minne. Kabla ya hapo mtoto awe ananyonyeshwa maziwa ya mama tu. Mtoto akifikisha umri wa miezi minne azoeshwe vyakula vya mchanganyiko, vilivyolainishwa kwa kiasi kidogo kidogo kwa muda wa miezi ya kwanza. Afikapo miezi sita awe ameanza kula vyakula vya familia vilivyopondwa pondwa, na taratibu kuongeza idadi ya milo kwa siku.

 

 

 

 

 

 

 

 



SWALI NA. 9: Nilipojifungua mtoto wangu wa mwisho titi langu moja lilivimba sana. Majirani wakanishauri nisimnyonyeshe mtoto wangu kutumia ziwa hilo. Nililiacha na kutumia titi moja tu. Je ni sahihi?

JIBU: Siyo sahihi kuacha kumyonyesha mtoto titi lenye uvimbe. Titi huvimba kama mtoto hakulinyonya vizuri na huendelea kuvimba hatimaye kuwa na jipu kama mtoto hatanyonyeshwa. Njia ya kupunguza uvimbe ni kuyakamua maziwa kwenye chombo ili kupunguza maziwa ndani ya titi lililovimba na kuendelea kumnyonyesha mtoto katika titi hilo. Uvimbe wa titi haudhuru maziwa ya mama na uvimbe hupungua haraka kama mtoto ataendelea kunyonyeshwa.

 

 

 

 

 

 



SWALI NA. 10: Ninatakiwa niendelee kumnyonyesha mtoto wangu mpaka awe na umri gani?

JIBU: Ili mtoto wako awe na afya nzuri unatakiwa uendelee kumnyonyesha kwa muda wa miaka miwili au zaidi. Unashauriwa sana usimwachishe ziwa mtoto wako kabla ya umri wa miaka miwili hata kama amezoea vizuri chakula cha familia. Maziwa ya mama bado yana umuhimu mkubwa katika umri huo.